The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesTaha [Taha] - Swahili translation - Rowad Translation Center
Surah Taha [Taha] Ayah 135 Location Maccah Number 20
Twa Ha![1]
Hatukukuteremshia Qur-ani ili upate mashaka.
Bali ni ukumbusho kwa mwenye kunyenyekea.
Ni uteremsho kutoka kwa aliyeumba ardhi na mbingu zilizo juu.
Arrahmani (Mwingi wa rehema), aliyeinuka juu ya Kiti cha Enzi.
Ni vyake vyote vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi, na vilivyo baina yake, na vilivyo chini ya ardhi.
Na ukinyanyua sauti kwa kusema, basi hakika Yeye anajua siri na chini zaidi kuliko siri.
Mwenyezi Mungu! Hakuna mungu yeyote isipokuwa Yeye. Yeye ana majina mazuri zaidi.
Na je, imekufikia hadithi ya Musa?
Alipouona moto, kwa hivyo akawaambia ahali zake: Ngojeni! Hakika mimi nimeuona moto, huenda nikawaletea kijinga kutoka humo, au nikapata uongofu kwenye moto huo.
Basi alipoufikia, akaitwa: Ewe Musa!
Hakika Mimi ndiye Mola wako Mlezi! Basi vua viatu vyako. Kwani uko katika bonde takatifu la 'Tuwa.
Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza yanayofunuliwa.
Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hakuna mungu isipokuwa Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na udumishe Swala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.
Hakika Saa itakuja bila ya shaka. Nimekaribia mno kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyoyafanya.
Kwa hivyo, kamwe asikuzuilie nayo yule ambaye haiamini na akafuata matamanio yake ukaja kuangamia.
Na nini hicho kilichomo mkononi mwako wa kulia, ewe Musa?
Akasema: Hii ni fimbo yangu; ninaiegemea na ninawaangushia majani kwayo kondoo na mbuzi wangu. Tena inanifaa kwa matumizi mengine.
Akasema: Itupe, ewe Musa!
Akaitupa. Mara ikawa nyoka anayekwenda mbio.
Akasema: Ikamate, wala usiogope! Tutairudisha hali yake ya kwanza.
Na uambatishe mkono wako kwenye ubavu, utatoka mweupe pasipo na madhara yoyote. Hiyo ni ishara nyingine.
Ili tukuonyeshe katika ishara zetu kubwa.
Nenda kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka.
(Musa) akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nikunjulie kifua changu.
Na nirahisishie kazi yangu hii.
Na lifungue fundo lililo katika ulimi wangu.
Wapate kufahamu maneno yangu.
Na nipe msaidizi katika ahali zangu.
Harun, kaka yangu.
Kwake yeye niongeze nguvu zangu.
Na mshirikishe katika jambo langu hili.
Ili tukutakase kwa wingi.
Na tukutaje kwa wingi.
Hakika Wewe unatuona vyema.
Akasema: Hakika Umeshapewa maombi yako, ewe Musa!
Na hakika tulikwishakufanyia hisani mara nyingine.
Pale tulipomfunulia mama yako yaliyofunuliwa,
Ya kuwa mtie katika kisanduku, na kisha kitie mtoni, na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu naye ni adui yake. Na nimekutilia mapenzi yanayotoka kwangu, na ili ulelewe machoni mwangu.
Dada yako alipokwenda na akasema: Je! Niwajulishe mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurejesha kwa mama yako ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ulimuua mtu, nasi tukakuokoa katika dhiki, na tukakujaribu kwa majaribio mengi. Ukakaa miaka kwa watu wa Madyana. Kisha ukaja kama ilivyokadiriwa, ewe Musa!
Na nimekuteua kwa ajili ya nafsi yangu.
Nenda, wewe na ndugu yako, pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka.
Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka.
Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.
Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.
Akasema: Msiogope! Hakika Mimi ni pamoja nanyi. Nasikia na ninaona.
Basi mwendeeni, na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola wako Mlezi! Basi waache Wana wa Israili watoke nasi, wala usiwaadhibu. Sisi tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na amani iwe juu ya atakayefuata uongofu.
Hakika tumefunuliwa sisi kwamba hakuna shaka adhabu itampata anayekadhibisha na akapuuza
(Firauni) akasema: Basi Mola wenu Mlezi ni nani, ewe Musa?
Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoa.
Akasema: Nini hali ya karne za kwanza?
Akasema: Elimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi katika Kitabu. Mola wangu Mlezi hapotei wala hasahau.
Ambaye amewafanyia ardhi kuwa tandiko, na akawapitishia humo njia, na akawateremshia kutoka mbinguni maji. Na kwa hayo tukatoa namna mbalimbali za mimea.
Kuleni, na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili.
Tumewaumba kutokana nayo (ardhi), na humo tutawarudisha, na tutawatoa kutoka humo mara nyengine.
Na hakika tulimwonyesha ishara zetu zote. Lakini alikadhibisha na akakataa.
Akasema: Ewe Musa! Hivyo umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?
Basi sisi hakika tutakuletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe, ambayo tusiivunje sisi wala wewe, mahali patakapokuwa sawa.
Akasema: Miadi yenu ni siku ya Sikukuu ya mapambo; na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri.
Basi Firauni akageuka akarudi, na akatengeneza hila yake, kisha akaja.
Musa akawaambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uongo, akaja kuwafutilia mbali kwa adhabu. Na hakika mwenye kuzua lazima ashindwe!
Basi wakazozana wenyewe kwa wenyewe kuhusiana na jambo lao hilo, na wakanong'ona kwa siri.
Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wao, na waondoe mila zenu zilizo bora kabisa.
Kwa hivyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu kweli kweli leo atakayeshinda.
Wakasema: Ewe Musa! Ima utupe wewe, au tuwe sisi ndio wa kwanza wa kutupa?
Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki! Kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinakwenda mbio.
Basi Musa akaingia hofu katika nafsi yake.
Tukasema: Usihofu! Hakika wewe ndiye utakayeshinda.
Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyoviunda. Hakika walivyounda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo.
Basi wachawi hao wakaangushwa chini wakasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa Harun na Musa!
(Firauni) akasema: Oh! Mmemuamini kabla ya mimi kuwapa ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi huu. Basi kwa yakini nitawakatakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutofautisha. Na lazima nitawatundika misalabani katika vigogo vya mitende, na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi ndiye mkali zaidi wa kuadhibu na kuiendeleza zaidi adhabu yake.
Wakasema: Hatutakupendelea wewe kuliko ishara waziwazi zilizotujia, na kuliko yule aliyetuumba. Basi hukumu utavyohukumu; kwani wewe hakika unahukumu tu haya ya maisha ya duniani.
Hakika sisi tumemuamini Mola wetu Mlezi ili atusamehe makosa yetu na uchawi uliotulazimisha kuufanya. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na Mwenye kudumu zaidi (katika kuadhibu).
Hakika atakayemjia Mola wake Mlezi naye ni mhalifu, basi kwa yakini, yake huyo ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi.
Na anayemjia Yeye naye ni Muumini na akatenda mema, basi hao watakuwa na daraja za juu.
Bustani za milele zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na hayo ndiyo malipo ya mwenye kujitakasa.
Na tulimfunulia Musa: Toka usiku na waja wangu, na uwapigie njia kavu baharini. Usihofu kukamatwa, wala usiogope.
Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake. Basi kikawafudikiza humo baharini kilichowafudikiza.
Na Firauni aliwapoteza watu wake wala hakuwaongoa.
Enyi Wana wa Israili! Hakika tuliwaokoa kutokana na adui yenu, na tukawaahidi upande wa kulia wa mlima na tukawateremshia Manna na Salwa.
Kuleni katika vitu vizuri hivyo tulivyowaruzuku, wala msiruke mipaka katika hayo, isije ikawashukia ghadhabu yangu. Na yule inayemshukia ghadhabu yangu basi huyo ameangamia.
Na hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia, na akaamini, na akatenda mema, kisha akaongoka.
Na nini kilichokutia haraka ukawaacha watu wako, ewe Musa?
Akasema: Hao wapo nyuma yangu wananifuata. Na nimefanya haraka kukujia, Mola wangu Mlezi, ili uridhike.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Sisi tumewatia mtihani watu wako baada yako, na Msamaria amewapoteza.
Basi Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu Mlezi hakuwaahidi ahadi nzuri? Je, umekuwa muda mrefu kwenu au mmetaka ghadhabu ya Mola wenu Mlezi iwashukie, ndiyo maana mkavunja miadi yangu?
Wakasema: Sisi hatukuvunja miadi yako kwa hiari yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya mapambo ya watu, basi tukaitupa. Na hivyo ndivyo alivyotupa yule Msamaria.
Na akawaundia ndama, kiwiliwili chenye sauti. Na wakasema: Huyu ndiye mungu wenu, na mungu wa Musa, lakini alisahau.
Je, hawakuona kuwa hakuwarudishia neno, wala kuwamilikia kudhuru wala kufaa?
Na hakika Harun alikwishawaambia kabla yake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmetiwa mtihanini tu kwa kitu hiki. Na kwa yakini Mola wenu Mlezi ni Arrahmani (Mwingi wa rehema). Basi nifuateni mimi, na tiini amri yangu!
Wakasema: Hatutaacha kumwabudu mpaka Musa atakaporejea kwetu.
(Musa) akasema: Ewe Harun! Ni nini kilichokuzuia, ulipowaona wamepotea?
Usinifuate. Je, umeasi amri yangu?
Akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu zangu, wala kichwa changu. Kwa hakika naliogopa usijesema: Umewatenganisha Wana wa Israili, na hukungojea kauli yangu.
(Musa) akasema: Ewe Msamaria! Unataka nini ?
Akasema: Niliona wasiyoyaona wao, nikachukua mkamato wa mkono katika athari za unyayo wa Mtume. Kisha nikaitupa. Na hivi ndivyo ilivyonielekeza nafsi yangu.
(Musa) akasema: Basi ondoka! Na kwa yakini utakuwa katika maisha ukisema: Usiniguse. Na hakika una ahadi kwako isiyovunjwa. Na mtazame huyo mungu wako uliyeendelea kumuabudu. Sisi kwa hakika tutamchoma moto, kisha tutamtawanya sawasawa baharini.
Hakika mungu wenu ni Allah (Mwenyezi Mungu) tu. Hakuna mungu isipokuwa Yeye. Amekienea kila kitu kwa elimu yake.
Namna hivi tunakuhadithia katika khabari za yaliyotangulia. Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha ya kukumbukwa.
Atakayeyapa mgongo, basi kwa yakini Siku ya Kiyama atabeba mzigo.
Wadumu humo. Na ni mzigo muovu kwao kuubeba Siku ya Kiyama!
Siku litakapopulizwa barugumu, na tukawakusanya wahalifu Siku hiyo, hali macho yao ni ya buluu.
Watanong'onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku kumi tu.
Sisi tunajua zaidi watakayoyasema, atakaposema mbora wao katika mwendo: Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu.
Na wanakuuliza habari za milima. Waambie: Mola wangu Mlezi ataivurugavuruga.
Na ataiacha tambarare, uwanda.
Hutaona humo mdidimio wowote wala muinuko.
Siku hiyo watamfuata muitaji huyo bila ya yeyote kumkengeuka. Na sauti zote zitamnyenyekea Arrahmani (Mwingi wa rehema). Basi hutasikia ila mnong'ono tu.
Siku hiyo uombezi hautafaa kitu, ila kwa atakayeruhusiwa na Arrahmani (Mwingi wa rehema) na akaridhia na maneno yake.
Yeye anajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao. Wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo.
Na zitadhalilika nyuso mbele ya Aliye Hai milele, Msimamia yote milele. Na atakuwa ameharibikiwa mwenye kubeba dhuluma.
Na anayetenda katika mema, naye ni Muumini, basi hatahofu kudhulumiwa wala kupunjwa.
Na namna hivi tumeiteremsha Qur-ani kwa Kiarabu, na tumekariri humo vitisho ili wapate kuogopa na kujilinda na iwaletee makumbusho.
Basi ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki. Wala usiifanyie haraka hii Qur-ani, kabla haujamalizika ufunuo wake. Na sema: Mola wangu Mlezi! Nizidishie elimu.
Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau, wala hatukupata kwake azimio kubwa.
Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu, isipokuwa Iblisi, alikataa.
Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo. Basi asiwatoe katika Bustani hii, mkaingia mashakani.
Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi.
Na hakika hutapata kiu humo wala hutapata joto.
Lakini Shetani alimtia wasiwasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujulishe mti wa kuishi maisha ya milele na ufalme usiokoma?
Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustanini. Na Adam akamuasi Mola wake Mlezi, na akapotea njia.
Kisha Mola wake Mlezi akamteua, na akamkubalia toba yake, na akamwongoa.
Akasema: Ondokeni humo nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukiwafikia uongofu kutoka kwangu basi atakayeufuata uongofu wangu, hatapotea wala hatataabika.
Na atakayeupa ukumbusho wangu mgongo, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa ni kipofu.
Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona vyema?
(Mwenyezi Mungu) atasema: Ndivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na vivyo hivyo leo utasahauliwa.
Na hivyo ndivyo tutakavyomlipa kila apitaye kiasi, na asiziamini ishara za Mola wake Mlezi. Na hakika adhabu ya Akhera ni kali zaidi, na inadumu zaidi.
Je, haikuwabainikia ni ngapi katika vizazi tuliviangamiza kabla yao, nao wanatembea katika maskani zao? Hakika katika hayo zimo ishara kwa wenye akili.
Na lau kuwa si neno lililokwishatangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi na muda uliowekwa, bila ya shaka ingefika adhabu (duniani).
Basi yavumilie haya wayasemayo. Na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla ya kuzama kwake, na nyakati za usiku pia umtakase, na nyakati za mwisho za mchana ili upate ya kukuridhisha.
Wala kamwe usivikodolee macho tulivyowastarehesha kwavyo baadhi ya watu miongoni mwao, kwa ajili ya mapambo ya duniani, ili tuwajaribu katika hivyo. Na riziki ya Mola wako Mlezi ni bora na yenye kudumu zaidi.
Na waamrishe ahali zako kuswali, na usubiri juu yake. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa ucha Mungu.
Na walisema: Kwa nini hakutuletea muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Je, haukuwajia ushahidi wazi wa yaliyo katika Vitabu vya mwanzo?
Na lau kuwa tuliwaangamiza kwa adhabu kabla yake, wangelisema: Ewe Mola wetu Mlezi! Kwa nini hukutuletea Mtume tukazifuata ishara zako kabla ya kudhalilika na kuhizika.
Sema: Kila mmoja anangoja. Basi ngojeni! Hivi karibuni mtajua ni akina nani ndio wenye njia sawa na ni nani aliyeongoka.