عربيEnglish

The Noble Qur'an Encyclopedia

Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languages

The Women [An-Nisa] - Swahili translation - Rowad Translation Center

Surah The Women [An-Nisa] Ayah 176 Location Madanah Number 4

Mwenyezi Mungu anawausia juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na wakiwa ni wanawake zaidi ya wawili, basi wana theluthi mbili za alichokiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na kwa wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi moja katika kile alichokiacha, ikiwa ana mtoto. Na ikiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wakawa wanamrithi, basi mama yake atapata theluthi moja. Na ikiwa ana ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alichousia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani kati yao aliyekaribu zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni sheria iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.

Nanyi mna nusu ya walichoacha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Lakini ikiwa wana mtoto, basi mna robo katika kile walichokiacha, baada ya wasia waliyousia au kulipa deni. Na wake zenu wana robo katika kile mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Lakini ikiwa mna mtoto, basi wana thumuni katika kile mlichokiacha, baada ya wasia mliousia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye kaka au dada, basi kila mmoja wao ana sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo, basi watashirikiana katika theluthi, baada ya wasia iliyousiwa au kulipa deni, pasi na kuleta madhara. Huu ndio wasia uliotoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mpole.

Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, naye ana adhabu ya kudhalilisha.

Mmeharamishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa kaka, na binti wa dada, na mama zenu waliowanyonyesha, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu waliozaliwa na wake zenu mliowaingilia. Ikiwa hamkuwaingilia, basi hakuna ubaya juu yenu. (Pia mmeharimishiwa) wake wa watoto wenu waliotoka katika migongo yenu. Na kuwaoa kwa pamoja dada wawili isipokuwa yale yaliyokwishapita. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.

Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake wa kiungwana Waumini, basi na aoe katika vijakazi Waumini iliowamiliki mikono yenu ya kulia. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe kwa wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kulingana na ada, wawe wanawake wema, si makahaba wala si mahawara. Na wanapoolewa kisha wakafanya uchafu basi adhabu yao itakuwa ni nusu ya adhabu waliyowekewa waungwana. Hayo ni kwa yule miongoni mwenu anayeogopa kuingia katika zinaa. Na mkisubiri, ndiyo bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.

Na mkihofia kuwepo mfarakano baina ya wawili hao, basi mtumeni mpatanishi kutoka kwa jamaa za mume, na mpatanishi kutoka kwa jamaa za mke. Ikiwa wanataka kutengeneza mambo, Mwenyezi Mungu ataleta maafikianao kati yao. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye habari zote.

Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema maadui zenu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mwenye kunusuru.

Je, hukuwaona wale wanaojitakasa nafsi zao? Bali Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye. Na hawatadhulumiwa hata kiasi cha kijiuzi kilicho ndani ya uwazi wa kokwa ya tende.

Basi miongoni mwao kuna yule aliyemwamini, na miongoni mwao kuna yule aliyemkufuru. Na Jahannamu inatosha kuwa ndio moto wenye mwako mkali.

Na hatukumtuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na lau pale walipozidhulumu nafsi zao, wangelikujia, wakamwomba Mwenyezi Mungu kuwafutia dhambi, na Mtume akawaombea kufutiwa dhambi, basi bila ya shaka wangelimkuta Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.

Hapana! Ninaapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye mwenye kuhukumu katika yale wanayohitilafiana, kisha wasipate uzito wowote katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wajisalimishe kujusalimisha kukamilifu.

Hiyo ndiyo fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kwamba ndiye Mwenye kujua vyema.

Yaliyokupata katika mazuri, basi ni kutokana na Mwenyezi Mungu. Na yaliyokusibu katika maovu, basi ni kutokana na nafsi yako. Nasi tumekutuma kwa watu uwe ni Mtume. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi.

Na wanasema: 'Tunatii.' Lakini wanapotoka kule uliko, kundi moja miongoni mwao hupanga njama usiku kinyume na unayoyasema. Na Mwenyezi Mungu anayaandika yote hayo wanayoyapangia njama za usiku. Basi wape mgongo, na umtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.

Basi pigana vita katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Hutwikwi isipokuwa nafsi yako tu. Na wahimize Waumini. Huenda Mwenyezi Mungu akayazuia mashambulizi ya wale waliokufuru. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mkali zaidi wa kushambulia, na Mkali zaidi wa kutesa.

Na mnapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo, au yarejesheni hayo hayo. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuhesabu kila kitu.

Basi mna nini mmekuwa makundi mawili kuhusiana na (habari ya) wanafiki, na ilhali Mwenyezi Mungu amewageuza kwa sababu ya yale waliyoyachuma? Je, mnataka kumwongoa yule ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza? Na mwenye kupotezwa na Mwenyezi Mungu, basi wewe hutapata njia yoyote kwa ajili yake.

Na haiwi Muumini kumuua Muumini isipokuwa kwa kukosea. Na mwenye kumuua Muumini kwa kukosea, basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa zake maiti, isipokuwa waiache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni wa kutoka kwa kaumu ambao ni maadui zenu, ilhali yeye ni Muumini, basi ni kwa kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa kaumu ambao kuna agano baina yenu na wao, basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiyepata, basi afunge miezi miwili mfululizo, iwe ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima kubwa.

Hivyo ni vyeo kutoka kwake, na kufutiwa dhambi, na rehema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kufuta dhambi, na Mwenye kurehemu sana.

Na unapokuwa miongoni mwao, na ukawasimamishia Swala, basi kundi moja miongoni mwao lisimame pamoja nawe, na wachukue silaha zao. Na watakapomaliza kusujudu, basi na wawe nyuma yenu, na lije kundi lingine ambalo halijaswali, na waswali pamoja nawe, nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walipenda wale waliokufuru lau mghafilike mbali na silaha zenu na mizigo yenu ili wawavamie mvamio wa mara moja. Wala hakuna ubaya juu yenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika, Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudunisha.

Na omba Mwenyezi Mungu kufutiwa dhambi. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.

Na anayetenda uovu au akaidhulumu nafsi yake, kisha akaomba kufutiwa dhambi kwa Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.

Na ni nani aliye bora zaidi kwa dini kuliko yule aliyeusilimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa ni mwema, na akafuata mila ya Ibrahim mnyoofu? Na Mwenyezi Mungu alimfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwandani.

Na wakitengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kutoka katika wasaa wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye hekima.

Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.

Bali Mwenyezi Mungu alimwinua kwenda kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Wanakuuliza hukumu ya kisheria, sema: Mwenyezi Mungu anawapa hukumu ya kisheria juu ya kalala (mtu aliyekufa bila ya kuacha mzazi wala mwana). Ikiwa mtu amekufa, naye hana mwana, lakini anaye dada, basi huyo atapata nusu ya alichokiacha. Naye (mwanamume) atamrithi (dada yake) ikiwa hana mwana. Na ikiwa wao ni madada wawili, basi watapata theluthi mbili za alichokiacha. Na wakiwa ndugu wanaume na wanawake, basi wa kiume atapata sehemu iliyo sawa na ya wa kike wawili. Mwenyezi Mungu anawabainishia ili msipotee. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.