The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Pen [Al-Qalam] - Swahili translation - Rowad Translation Center
Surah The Pen [Al-Qalam] Ayah 52 Location Maccah Number 68
Nuun. Ninaapa kwa kalamu na yale wayaandikayo.[1]
Kwa neema ya Mola wako Mlezi wewe si mwendawazimu.
Na kwa hakika wewe una malipo yasiyokatika.
Na hakika wewe una tabia tukufu.
Karibu utaona, na wao wataona.
Ni nani kati yenu aliyepandwa na wazimu.
Hakika Mola wako Mlezi ndiye ajuaye zaidi ni nani aliyeipotea njia yake, na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka.
Basi usiwatii wanaokadhibisha.
Walitamani lau ungelainisha ili nao wakulainishie.
Wala usimtii kila mwingi wa kuapa, anayedharauliwa.
Mwenye kukejeli mno, anayetangatanga akieneza maneno ya kufitini.
Mwenye kuzuia mno heri, dhalimu, mwingi wa madhambi.
Mkatili, na juu ya hayo, ni mshari aliyejipachika tu.
Ati kwa kuwa ana mali na watoto!
Anaposomewa Aya zetu, husema: "(Hizi ni) simulizi za uongo za watu wa zamani!"
Tutamtia alama kwenye pua yake.
Hakika tuliwajaribu hawa kama tulivyowajaribu wale wenye shamba, walipoapa kwamba lazima watayavuna mazao yake itakapokuwa asubuhi.
Wala hawakusema: Mwenyezi Mungu akipenda!
Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako Mlezi, nao wamelala!
Likawa kama usiku wa giza.
Kisha asubuhi wakaitana.
Ya kwamba: "Nendeni mapema kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna."
Basi walikwenda huku wananong'onezana.
Ya kuwa: "Leo kamwe masikini mmoja asikuingilieni."
Na walikwenda asubuhi, nao wameshikilia azimio hilo.
Basi walipoliona, wakasema: Hakika tumepotea!
Bali tumenyimwa!
Mbora wao akasema: Sikukwambieni, kwa nini hamumtakasi Mwenyezi Mungu?
Wakasema: Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu.
Basi wakaelekeana kulaumiana wao kwa wao.
Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa tumeikiuka mipaka!
Asaa Mola wetu Mlezi akatubadilishia lililo bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
Namna hivi yanakuwa mateso, na bila ya shaka mateso ya Akhera ni makubwa zaidi, laiti wangelijua!
Hakika wacha Mungu watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao Mlezi.
Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu?
Mna nini? Mnahukumu vipi?
Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma?
Kuwa mtapata humo mnayoyapenda?
Au mnazo ahadi za viapo juu yetu za kufika Siku ya Kiyama ya kuwa hakika mtapata kila mnayojihukumia?
Waulize: Ni nani miongoni mwao dhamini wa haya?
Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanasema kweli.
Siku utakapowekwa wazi muundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza
Macho yao yatainama chini, fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipokuwa wazima.
Basi niache na wanaokadhibisha maneno haya! Tutawavutia kidogo kidogo kutokea mahali wasipopajua.
Na ninawapururia muhula; hakika hila zangu ni imara.
Au unawaomba ujira, na wao wanaemewa na gharama hiyo?
Au iko kwao siri, basi wao wanaiandika?
Basi ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, wala usiwe kama mmezwa na samaki, aliponadi naye kazongwa.
Kama isingelimfikia neema kutoka kwa Mola wake Mlezi, bila ya shaka angelitupwa ufukweni naye ni mwenye kulaumiwa.
Lakini Mola wake Mlezi alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema.
Na waliokufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanaposikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu.
Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.