The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesHe Frowned [Abasa] - Swahili translation - Rowad Translation Center
Surah He Frowned [Abasa] Ayah 42 Location Maccah Number 80
Alikunja kipaji na akageuka mbali.
Kwa sababu alimjia kipofu!
Na nini kitakachokujulisha pengine yeye atatakasika?
Au atawaidhika, na mawaidha yamfae?
Ama ajionaye hana haja,
Wewe ndiyo unamshughulikia?
Na si juu yako kama hakutakasika.
Ama anayekujia kwa juhudi.
Naye anaogopa,
Ndiyo wewe unampuuza?
Sivyo hivyo! Huku ni kukumbushana.
Basi anayependa akumbuke.
Yamo katika kurasa zilizoheshimiwa.
Zilizoinuliwa, zilizotakaswa.
Zimo mikononi mwa Malaika waandishi,
Watukufu, wema.
Ameangamia mwanadamu! Nini kinachomkufurisha?
Kwa kitu gani amemuumba?
Kwa tone la manii, amemuumba na akamkadiria.
Kisha akamsahilishia njia.
Kisha akamfisha, akamtia kaburini.
Kisha apendapo atamfufua.
La! Hajamaliza aliyomuamuru.
Hebu mtu na atazame chakula chake.
Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu.
Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu.
Kisha tukaotesha humo nafaka.
Na zabibu, na mimea ya majani.
Na mizaituni, na mitende.
Na bustani zenye miti iliyosongana barabara.
Na matunda, na malisho ya wanyama.
Kwa manufaa yenu na mifugo yenu.
Basi utakapokuja ukelele.
Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye.
Na mamaye na babaye.
Na mkewe na wanawe.
Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha.
Siku hiyo ziko nyuso zitakazonawiri.
Zitacheka, zitachangamka.
Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi.
Giza totoro litazifunika.
Hao ndio makafiri watenda maovu.